Jengo La TCRA Makao Makuu |
Kitendo cha kufunga namba hizo tangu Juni Mosi mwaka huu, kimewapa hofu wananchi waliokuwa wakitumia laini bila kuzisajili.
Kutokana na hofu hiyo, watumiaji wa laini ‘bubu’ yaani zisizotambulika TCRA wamejitokeza kwa wingi kwa mawakala wa mitandao mbalimbali kusajili.
Jana MTANZANIA ilitembelea vituo mbalimbali vya mawakala wa usajili jijini Dar es Salaam na kushuhudia kuwapo na watu wengi isivyo kawaida wakisajiliwa namba zao.
Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti, walisema kuwa hawakuona umuhimu wa kusajili namba hizo kwa sababu zilikuwa zikiendelea kutumika bila matatizo.
Alphonce Njomela ni miongoni mwa watumiaji wa namba zisizosajiliwa, ambapo alisema kuwa baada ya kuona namba zikifungwa zisizotumika zaidi ya miezi mitatu, amekuwa na hofu.
“Awali tuliambiwa tusajili ili kuzuia wizi na hata simu ikiibiwa haitatumika baada ya kutoa taarifa lakini hatukuona matunda yoyote, nikaamua kuendelea kutumia bila kusajili,” alisema.
Mtumiaji mwingine aliyejitambulisha Motondi Juma, alisema namba yake ya awali alisajili lakini baada ya kuibiwa simu na kununua nyingine hakuona umuhimu wa kusajili.
Alisema kuwa licha ya kuwapo na tishio la TCRA kuzifunga amelazimika kusajili, ili kunusuru namba za ndugu na marafiki kwani kuzipata si rahisi.
Vile vile alisema kuwa amelazimika kusajili ili kupata huduma za kifedha zinazotolewa kupitia mitandao ya simu.